Salamu Zangu Unavyotesa Bongo!
Wimbo wa Salamu zangu uliotungwa na Bi Irene Sanga na kuimbwa naye kwa kushirikiana na Mrisho mpoto umetokea kufunika mno katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania, hasa kutokana na misemo yake isiyochosha kusikiliza!
Hebu usome hapa mashairi yake...
Kiitikio
Taifa liwapo na huzuni lazima wote tufunge mikanda kiunoni ili matanga yaishe upesi, majanga yanapozidi kimo mioyo ya wanadamu huota kutu hizo ni salam zangu...
Pepo hazina sifa ila pawapo Jehanamu, uzuri ni kipimo cha ubaya, kwani kiumbe chenye uhai na mauti huongozwa na tamaa salam zangu kwako eeehh!
Ubeti I:
Mpendwa mjomba tumetenganishwa na ukuta sidhani kama utatembelea tena kama msimu uliopita, japo kwa sasa utakuwa adimu pokea salamu zangu!
Ukienda msibani aliyefiwa utamjua, atakuwa amevaa tofauti na wenzake na machozi yasokauka... Mimi najua ni wewe mfiwa alo na huzuni msiba wetu kuubeba!
Ala moja haikai panga mbili, gimba lisilo akili Waswahili husema ni gogo, taja magogo yote la mbuyu si la mvule, aah funzo la mjinga ni taabu, gome la udi si la mnuka uvundo, isiyokuwasha hujailamba, pokea salamu zangu mjomba!
Ola wendako kabla hujafika, osha uso ndipo ua nje, pa shoka hapaingii kisu, tukifunga mikanda matanga yata isha upesi kwani zindiko la mwoga ni kemi, ukistahi mke ndugu huzai naye, kumbuka vijana ni samadi ya Taifa hili hizi ni salam zangu kwako mjomba!
Mjomba maisha ni sahani iliyojaa kila aina ya uchafu, umeibeba, dudu liumalo usilipe kidole, enda na uchao, usende na uchwao, kichwa cha nyoka hakibandiki mtungi ati, kosa halitengezi kosa , mchunga peku hapendi ila hana viatu, sikufundishi mjomba ila ni salam zangu kwako!
Mwenda mbio kaagana na nyonga, umesha agana na nyonga weye? Usiukubali Utanzania na kutukuza Uingereza, usifikiri kwa lugha za kigeni, fikra sahihi, huja kwa lugha sahihi!
Rushwa, rushwa ni wimbo wa sumu uliotapakaa kwenye ubongo wa kila mwana Taifa hili, tubadilishie wimbo huu tafadhali, turudishie nyimbo zetu za ushujaa, nyimbo za makuzi na jando la Taifa!
Nakuomba jaribu kula majalalani na watoto wa mitaani badala ya kusema this country bwana is very poor? Waonee huruma wajawazito wakiwa wamelala mzungu wa nne kule Amana huku matumbo ya mama hawa yakisubiri mgomo wa madaktari uishe, wengine wakilia kwa kupoteza vichanga vyao
Kiitikio tena!
Ubeti II:
Wapokee masufuria ya moto mama ntilie wakiwa wanafukuzwa na Wagambo wamurike mapolisi wenye madaraka mkononi wakiwahukumu raia kwa makofi kabla hakimu hajasoma hukumu, watoe wafungwa waliofungwa kwa hila na chuki binafsi, sikufundishi mjomba hizo ni salam zangu kwako!
Unakazi mjomba, kumbusha jopo lako wametupima viatu mwaka huu baada ya miaka mitano watatuuliza mlikuwa mnataka viatu vya aina gani?
Maneno mengi hayajengi ghorofa, hili ni ombi langu la mwisho kwako, vibwaya, vibwaya viweke ghalani, siku yake utavikumbuka ili tucheze ngoma yetu wanayoiita ngoma ya kishenzi, visima vya kale havifukiwi mjomba, salamu zangu kwako, ndimi pangu pakavu nakusalimia!
Kiitikio tena!
1 Comments:
Mzawa,
Hebu naomba ukikutana na hawa watu unifikishie salamu zangu.
Post a Comment
<< Home