Tuesday, November 21, 2006

Ditopile Alia na Rais Kikwete, Shein!



Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora Ndugu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri wamelaani kitendo cha vingozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Rais Jakaya Kikwete na Makamu wake Dk Ally Mohamed Shein kwenda kutoa rambirambi kwa familia ya aliyekuwa dereva wa daladala Hassan Mbonde anayedaiwa kuuawa na bw Ditopile!

Mawakili wa Ditopile wakiongea kwa niaba yake walisema kuwa kitendo cha viongozi hao kwenda kuhani kwa familia ya dereva huyo kwa ving'ora na promo za nguvu kunatoa sura ya kumtia hatiani Dito kabla ya mahakama kuthibitisha hilo, hivyo kuitaka Mahakama kuzuia rambirambi hizo mara moja!

Hata hivyo Mahakama hiyo ya Kisutu imelitosa ombi hilo, kwa kile kilichoelezwa kuwa mahakama haifanyii kazi mambo yanayotokea mitaani, Dito amerudishwa tena rumande hadi kesi itakapotajwa tena!

na Irene Mark
MWANASHERIA maarufu wa kimataifa, Nimrod Mkono, amechukua jukumu la kuwa kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile - Mzuzuri, anayekabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Mkono, ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), sasa anaungana na mawakili wengine wanne. Mawakili hao ni Dk. Ringo Tenga, Cuthbert Tenga, Rosan Mbwambo, na Samuel Mapande.
Jana Mkono alisimama mahakamani Kisutu, na kuanza kumtetea mteja wake, akianza na hoja ya kupinga viongozi mbalimbali wa serikali, kwenda kuhani nyumbani kwa marehemu, Hassan Mbonde, ambaye alikuwa dereva wa daladala.
Alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Michael Luguru, kwamba kitendo cha viongozi wa serikali kwenda nyumbani kwa mfiwa si kumtendea haki mteja wao, kwa kuwa anakuwa amekwisha kuhukumiwa kwamba ameua.
“Viongozi wa nchi wanaokwenda kumwona mfiwa na kutoa rambirambi wanatupa wasiwasi kama haki itatendeka.
“Hivi Jaji Mkuu akiamua kwenda kutoa pole, itakuwaje? Spika akienda, hata wewe Mheshimiwa hakimu, itakuwaje?”
“Wanakwenda na vinolinoli (ving’ora) na kutoa pole na fedha, vyombo vya habari vinaandika, hii inaweza kusababisha haki kutotendeka kwa mtuhumiwa, mahakama iwapige marufuku hawa,” alidai Mkono.
Alivishukuru vyombo vya habari kwa kuandika ziara za viongozi wa serikali nyumbani kwa mfiwa, kwa kuwa bila hivyo jamii isingefahamu kwamba familia ya marehemu inatembelewa na viongozi hao.
Mkono alisema kitendo kilichofanywa na viongozi wa serikali, ni ukiukwaji wa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ibara hiyo inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria, na ni marufuku mtu kubaguliwa kwa namna yoyote ile.
Alisema ziara hizo zimefanywa nyumbani kwa wazazi na familia ya wafiwa pekee, na kwamba ingekuwa haki kama viongozi hao pia wangemtembelea mteja wake mahabusu ambako anaendelea kushikiliwa.
Baadhi ya viongozi waliokwenda kuhani ni Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ambaye alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete na kutoa ubani wa sh 500,000.
Pia Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein; Meya wa Kinondoni, Salum Londa; na wengine wengi, wamekwisha kwenda kuhani.
“Kila siku matukio ya kuuawa yanatokea, lakini hatuwaoni kwenda…basi kama wanataka kwenda wachukue likizo au waende kwa siri, huu ni ukiukwaji wa Katiba,” alidai Mkono.
Akijibu hoja za wakili huyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Kenyella, alidai kwamba mahakama haifanyi kazi kwa kusikiliza maneno ya watu au matendo ya viongozi wa serikali.
Alimtaka wakili huyo kutokuwa na wasiwasi juu ya utendaji wa haki.
Baada ya hoja na majibu ya pande zote, Hakimu Luguru, alisema kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji, haiwezi kutoa agizo lolote.
Alisema malalamiko ya wakili huyo wa utetezi yanawekwa katika maandishi, yakaamuliwe na Mahakama Kuu.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 4, mwaka huu, itakapotajwa tena. Upelelezi haujakamilika.
Ilidaiwa kwamba Novemba 14, mwaka huu, kwenye makutano ya Barabara ya Bagamoyo na Kawe, Dar es Salaam, Ditopile-Mzuzuri, alimuua Hassan Mbonde, kwa kumpiga risasi.
Kama ilivyokuwa wiki mbili zilizopita mahakamani hapo, jana Ditopile-Mzuzuri, alikuwa mnyonge, na muda wote alionekana kujiinamia.
Mkono wake wa kulia ambao inadaiwa kwamba aliumizwa kwenye eneo la tukio, haukuwa na bandeji; hali iliyofanya kovu kubwa lionekane.
Jana alivaa shati la kitenge lenye rangi ya kijani kikavu, suruali nyeusi na balaghashia nyeupe.
Kuwapo kwa Mkono katika kesi hiyo, kunaongeza mvuto, kwani ni nadra mno kwa wakili huyo kusimama katika kesi za kawaida.
Kesi ambayo aliweza kuonekana ni ile ya kumtetea mfanyabiashara, Valambia.
Mkono anatambuliwa na kuheshimika kimataifa, kama mmoja wa mawakili maarufu na wenye mafanikio makubwa katika fani ya sheria.
Hivi karibuni alipokea tuzo ya kimataifa nchini Uingereza.
Wakati huo huo, Mkono alitoa hoja hizo mahakamani, Mnajimu Sheikh Yahya Hussein, juzi aliitembelea familia ya marehemu Mbonde na kuahidi kumtibu kiharusi, mama wa marehemu.
“Wameonyesha kufarijika sana kwa michango mbalimbali iliyotolewa na viongozi wa kiserikali, kisiasa, kidini na watu binafsi…kama mtumishi wa Kurani
nimewaomba na wameniruhusu niwapeleke Hijja watu wawili kutoka kwenye familia yao akiwamo baba mzazi wa marehemu.
“Maandalizi kwa ajili ya ahadi hiyo nimeanza kuyatekeleza leo (jana),” alisema.

http://www.freemedia.co.tz/daima/2006/11/21/habari1.php

0 Comments:

Post a Comment

<< Home