Friday, November 24, 2006

Kuna Ukweli katika Hili?!

Kuna uvumi huku Bongo unadai kuwa uhusiano wa Jay Z na Beyonce eti hauko sawa kwa sasa, ambapo Beyonce 'analiwa' na Usher Raymonds huku Jay Z naye 'anamla' Rihanna, eti wachunguzi wa mambo hebu nisaidieni katika hilo!

Beyonce Na Usher - video powered by Metacafe

Kanisa la St Peter Osterbay


Kanisa hili lipo Osterbay, Dar jirani kabisa na Makao Makuu ya Usalama wa Taifa, historia ya kipekee kwa kanisa hili ni ibada zake kuhudhuriwa mno na viongozi wa Serikali ya Tanzania na hata maofisa wa balozi mbalimbali zilizopo Bongo!
Hapa ndo hayati Mwl Julius Nyerere alikuwa na sehemu yake maalum, si unajua tena huyu alikuwa neva miss katika Ibada!

Viwanja vya Disko Siku hizi Kibao!


Siku hizi 'viwanja' vya disko vimekuwa vingi sana Bongo tofauti na zamani, Kuna JJ Club, Bar One, Garden Bistro, Arabella na vingine kibao, kila wikiendi ni kuruka kwanja kwa kwenda mbele... Zamani ilikuwa Billz sijui na Mambo Club, mtanisaidia zaidi wadau!
Hiyo hapo pichani ni kiwanja cha Garden Bistro kiko mitaa ya Masaki!

Thursday, November 23, 2006

Ray C Anakuja na Albamu ya Pili!


Mtoto wa kike Rehema Chalamila au Ray C, aliwahi kuvuma sana redioni akiwa mtangazaji wa East Africa Radio (Radio One Channel three)na baadaye Clouds FM amenitumia Email ya kunihabarisha kuwa albamu yake imeshaiva, hivyo anatarajia kuitoa siku si nyingi!

Hebu nawe icheki barua pepe yake hapa chini...
Mambo vipi? Albamu yangu ina nyimbo kumi na moja nakutajia baadhi ya majina...

Tabasamu lako (REGGAE)
Wawili (ZOUK)
Siangalii nyuma feat Dgritty mdogo wake Loon
Nilikutamani feat TID
Mapenzi ya kweli
Kama wanipenda feat Pfunk
Sogea Sogea
Sogea sogea remix
Sugadaddy
Kwa ajili yako feat Nako 2 Nako
Niacheni

Album itatoka mwezi ujao mwanzoni, nimerekodi studio tofauti ambazo ni Metro Studio, Mandugu Digital na Bongo Records!

Juma Nature Ajitoa TMK Wanaume Family!


Mwanamuziki mahiri wa Bongo Flava, Juma Kassim au Sir Nature ambaye hivi karibuni aliwania moja ya tuzo za MTV Base maeripotiwa kujitoa katika kundi lake Wanaume TMK baada ya kutokea kutoelewana kati yao!
Meneja wa kundi hilo, Said Fella alithibitisha kujitoa kwa msanii huyo akiwa na wasanii wengine wa kundi hilo, D Chief, Dolo na Luten Kalama, kwa kile alichokieleza kuwa ni tabia ya ubinafsi ya wasanii hao!
Wasanii wengine waliobaki, wametanabaisha kuwa, kuondoka kwa wasanii hao hakuwafanyi kutoendelea na 'kukamua' hivyo wametuhakikishia kuwa yale 'mapanga shaa' yataendelea!
Hata hivyo kuna fununu kuwa wasanii hao waliojitoa katika kundi hilo, wanatarajia kuungana na Inspekta Haroun au Babu na kuibuka na kundi lao jipya linalotarajia kuanza mambo yake hivi karubini, isitoshe wimbo mpya wa Nature na Inspekta uitwao Hakuna Kuremba unatarajia kutoka hivi karibuni!

Tuesday, November 21, 2006

Ditopile Alia na Rais Kikwete, Shein!



Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora Ndugu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri wamelaani kitendo cha vingozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Rais Jakaya Kikwete na Makamu wake Dk Ally Mohamed Shein kwenda kutoa rambirambi kwa familia ya aliyekuwa dereva wa daladala Hassan Mbonde anayedaiwa kuuawa na bw Ditopile!

Mawakili wa Ditopile wakiongea kwa niaba yake walisema kuwa kitendo cha viongozi hao kwenda kuhani kwa familia ya dereva huyo kwa ving'ora na promo za nguvu kunatoa sura ya kumtia hatiani Dito kabla ya mahakama kuthibitisha hilo, hivyo kuitaka Mahakama kuzuia rambirambi hizo mara moja!

Hata hivyo Mahakama hiyo ya Kisutu imelitosa ombi hilo, kwa kile kilichoelezwa kuwa mahakama haifanyii kazi mambo yanayotokea mitaani, Dito amerudishwa tena rumande hadi kesi itakapotajwa tena!

na Irene Mark
MWANASHERIA maarufu wa kimataifa, Nimrod Mkono, amechukua jukumu la kuwa kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile - Mzuzuri, anayekabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Mkono, ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), sasa anaungana na mawakili wengine wanne. Mawakili hao ni Dk. Ringo Tenga, Cuthbert Tenga, Rosan Mbwambo, na Samuel Mapande.
Jana Mkono alisimama mahakamani Kisutu, na kuanza kumtetea mteja wake, akianza na hoja ya kupinga viongozi mbalimbali wa serikali, kwenda kuhani nyumbani kwa marehemu, Hassan Mbonde, ambaye alikuwa dereva wa daladala.
Alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Michael Luguru, kwamba kitendo cha viongozi wa serikali kwenda nyumbani kwa mfiwa si kumtendea haki mteja wao, kwa kuwa anakuwa amekwisha kuhukumiwa kwamba ameua.
“Viongozi wa nchi wanaokwenda kumwona mfiwa na kutoa rambirambi wanatupa wasiwasi kama haki itatendeka.
“Hivi Jaji Mkuu akiamua kwenda kutoa pole, itakuwaje? Spika akienda, hata wewe Mheshimiwa hakimu, itakuwaje?”
“Wanakwenda na vinolinoli (ving’ora) na kutoa pole na fedha, vyombo vya habari vinaandika, hii inaweza kusababisha haki kutotendeka kwa mtuhumiwa, mahakama iwapige marufuku hawa,” alidai Mkono.
Alivishukuru vyombo vya habari kwa kuandika ziara za viongozi wa serikali nyumbani kwa mfiwa, kwa kuwa bila hivyo jamii isingefahamu kwamba familia ya marehemu inatembelewa na viongozi hao.
Mkono alisema kitendo kilichofanywa na viongozi wa serikali, ni ukiukwaji wa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ibara hiyo inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria, na ni marufuku mtu kubaguliwa kwa namna yoyote ile.
Alisema ziara hizo zimefanywa nyumbani kwa wazazi na familia ya wafiwa pekee, na kwamba ingekuwa haki kama viongozi hao pia wangemtembelea mteja wake mahabusu ambako anaendelea kushikiliwa.
Baadhi ya viongozi waliokwenda kuhani ni Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ambaye alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete na kutoa ubani wa sh 500,000.
Pia Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein; Meya wa Kinondoni, Salum Londa; na wengine wengi, wamekwisha kwenda kuhani.
“Kila siku matukio ya kuuawa yanatokea, lakini hatuwaoni kwenda…basi kama wanataka kwenda wachukue likizo au waende kwa siri, huu ni ukiukwaji wa Katiba,” alidai Mkono.
Akijibu hoja za wakili huyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Kenyella, alidai kwamba mahakama haifanyi kazi kwa kusikiliza maneno ya watu au matendo ya viongozi wa serikali.
Alimtaka wakili huyo kutokuwa na wasiwasi juu ya utendaji wa haki.
Baada ya hoja na majibu ya pande zote, Hakimu Luguru, alisema kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji, haiwezi kutoa agizo lolote.
Alisema malalamiko ya wakili huyo wa utetezi yanawekwa katika maandishi, yakaamuliwe na Mahakama Kuu.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 4, mwaka huu, itakapotajwa tena. Upelelezi haujakamilika.
Ilidaiwa kwamba Novemba 14, mwaka huu, kwenye makutano ya Barabara ya Bagamoyo na Kawe, Dar es Salaam, Ditopile-Mzuzuri, alimuua Hassan Mbonde, kwa kumpiga risasi.
Kama ilivyokuwa wiki mbili zilizopita mahakamani hapo, jana Ditopile-Mzuzuri, alikuwa mnyonge, na muda wote alionekana kujiinamia.
Mkono wake wa kulia ambao inadaiwa kwamba aliumizwa kwenye eneo la tukio, haukuwa na bandeji; hali iliyofanya kovu kubwa lionekane.
Jana alivaa shati la kitenge lenye rangi ya kijani kikavu, suruali nyeusi na balaghashia nyeupe.
Kuwapo kwa Mkono katika kesi hiyo, kunaongeza mvuto, kwani ni nadra mno kwa wakili huyo kusimama katika kesi za kawaida.
Kesi ambayo aliweza kuonekana ni ile ya kumtetea mfanyabiashara, Valambia.
Mkono anatambuliwa na kuheshimika kimataifa, kama mmoja wa mawakili maarufu na wenye mafanikio makubwa katika fani ya sheria.
Hivi karibuni alipokea tuzo ya kimataifa nchini Uingereza.
Wakati huo huo, Mkono alitoa hoja hizo mahakamani, Mnajimu Sheikh Yahya Hussein, juzi aliitembelea familia ya marehemu Mbonde na kuahidi kumtibu kiharusi, mama wa marehemu.
“Wameonyesha kufarijika sana kwa michango mbalimbali iliyotolewa na viongozi wa kiserikali, kisiasa, kidini na watu binafsi…kama mtumishi wa Kurani
nimewaomba na wameniruhusu niwapeleke Hijja watu wawili kutoka kwenye familia yao akiwamo baba mzazi wa marehemu.
“Maandalizi kwa ajili ya ahadi hiyo nimeanza kuyatekeleza leo (jana),” alisema.

http://www.freemedia.co.tz/daima/2006/11/21/habari1.php

Sunday, November 19, 2006

Ajali!


Mzee huyu ambaye jina lake halikutambulika jana mida ya saa kumi hivi alipata ajali ya gari wakati akivuka barabara ya Lumumba maeneo ya Mnazi Mmoja, Dar! Aliteguka kiuno na kupasuka kichwa, dereva alijikata bila kutoa msaada wowote, lakini namba zilidakwa na wasamalia wema... Mzee akakimbizwa Muhimbili kwa matibabu!
Hapa baadhi ya watu wakimshuhudia mzee huyo baada ya kugongwa!

Friday, November 17, 2006

Hii Hapa Mdau!


Kuna mdau mmoja aliniomba chanzo cha habari ya Amina Chifupa kutishiwa kuuawa mara baada ya kutangaza wazi azma yake ya kufyatua mabomu ya wauza unga!

Chifupa atishiwa kuuawa

2006-11-16 09:03:34
Na Rosemary Mirondo na Beatrice Philemon
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Bi. Amina Chifupa, ametishiwa kuuawa na watu wasiojulikana kupitia simu yake ya mkononi.

Madai ya mbunge huyu aliyatoa jana alipozungumza na waandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka Dodoma alikokuwa akihudhuria kikao cha Bunge kilichomalizika jana.
Alisema amepokea vitisho kupitia vijikaratasi alivyoandikiwa akiwa ndani ya ukumbi wa Bunge, vikimuonya aachane na suala la wauza unga.
’’Sambamba na ujumbe huo, kupitia simu yangu ya mkononi nilitumiwa ujumbe mfupi wa maneno wa kunitishia kuniua.
’’Mbali na hayo, ndani ya ukumbi wa Bunge kwenyewe nimepokea ujumbe wa vikaratasi visivyo na majina vikisema kwamba ninajifanya najua kuongea’’, aliongeza kusema mbunge huyo ambaye alisisitiza bado hatetereki kwa vitisho hivyo.
Ujumbe mwingine unasema ”we Amina wewe acha wewe, usijifanye unajua sana, ukiwa kwenye jumba la vioo usirushe mawe wakati na wewe umo ndani, tunaanza kukuchunguza kuanzia leo unapata wapi pesa, ni SISI USALAMA WA TAIFA
Hivi wewe Amina unajiona wewe ni msafi sana? Au kwa kuwa sisi tumekaa kimya.
Wewe ni mchafu sana , na sisi tukiamua kuanza kukuchafua hapatakalika hapa. Dawa yako iko jikoni inachemka, ndio utajua sisi ni nani umeyataka mwenyewe usimlaumu mtu. Wameshindwa wakongwe wewe mtoto wa juzi.
Aidha Bi.Amina alipigiwa simu inayoonyesha kutoka nje ambayo ilisomeka call kwenye simu yake yenye matusi ya nguoni yakimuonya aache kuropoka.
Vitisho dhidi ya mbunge huyu jasiri na chipukizi, vimekuja siku moja tu baada ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai nchini, Bw.Robert Manumba kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litamlinda na lipo tayari kupokea taarifa zinazohusu vinara wa uuzaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini.
Aidha, Bi. Amina alisema amepokea simu kutoka kwa mtu aliyejitaja kuwa ni polisi, akimuonya asiongee na mtu yeyote kuhusu suala hilo, mpaka atakapotoka bungeni na kumshauri mara atakapotoka Dodoma aende moja kwa moja kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Bw. Robert Manumba, kuonana naye.
Hata hivyo, Bi. Amina hakutaka kutaja jina la polisi huyo.
Bi. Amina alisema pamoja na kupokea vitisho hivyo, hataacha kufichua wafanyabiashara hao kwa sababu wanachangia kuwaangamiza vijana ambao ni taifa la kesho.
Alisema baada ya kutangaza bungeni kuwa yupo tayari kuwafichua vigogo wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ameanza kupata ushirikiano kutoka kwa wabunge wachache wanaochukizwa na biashara hiyo.
Nipashe ilipoongea na Kamishna Manumba jana kuhusu vitisho anavyopokea Mbunge huyo, alisema yeye hajapata taarifa zozote mbali na kusema kuwa suala hilo linahitaji kushughulikiwa kitaalamu.
Hata hivyo, alisema kwa sasa anaweza kuwasiliana na kituo cha polisi Dodoma au kikosi cha kuzuia madawa ya kulevya.
”Pamoja na ujasiri wa Mbunge huyo, pia tunahitaji watu wengine wajitokeze kutoa majina ya wafanyabiashara hao ili tuweze kutokomeza biashara hiyo inayoleta madhara nchini,” alisema Bw. Manumba.
Kamishna Manumba alisema kuwa ili kuweza kukabiliana na biashara hiyo nchini, unahitajika ushirikiano kutoka serikalini na watu binafsi kwani suala hilo litashughulikiwa kwa siri kwa ajili ya kuwalinda watoa taarifa.
”Serikali ishirikiane kupiga vita suala hilo kisiasa na sisi tutalishughulikia kitaaluma,” alisema Kamishna Manumba.
Alisema hilo ni tatizo la kimataifa hivyo inakuwa ni vugumu kuwabaini vigogo halisi wanaohusika na kilimo na kutengeneza madawa hayo kwani hapa nchini wanaohusika na madawa ya kulevya ni mawakala.
Alisema kuwa wazalishaji wakubwa wapo nchi za nje kama Mashariki ya Kati, Mashariki ya Mbali, Latin America na Afghanstan.
Aliongeza kuwa kama serikali za nchi za Afrika na Bara la Ulaya zitakuwa imara, vyombo vya serikali vitaweza kufanyakazi zake vizuri katika kuweka mikakati ya kupambana hatimaye kupunguza tatizo hilo la madawa ya kulevya.
Hata hivyo, Kamishna Manumba alisema kuwa hadi sasa hawajapata ushahidi unaoonyesha kwamba vigogo wanaotoka serikalini au taasisi wanashiriki katika uuzaji wa dawa za kulevya ila wamebaini kuwa kuna wafanyabiashara wakubwa ndio wanaoongoza kuingiza madawa ya kulevya nchini kama mawakala.

SOURCE: Nipashe

Thursday, November 16, 2006

Amina Chifupa Atishiwa Kuuawa!


Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Bi Amina Chifupa Mpakanjia amepata vitisho kadhaa vya kuuawa kutoka kwa watu wasiojulikana ikiwa ni baada ya kuahidi kuwataja VIGOGO kadhaa wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini!

Bi Chifupa alitoa ahadi hiyo Bungeni Dodoma na kuungwa mkono na Mkurugenzi wa makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba anayemsubiri kwa hamu ofisini kwake Mbunge huyo kwa ajili ya kumpatia orodha hiyo!

Salamu Zangu Unavyotesa Bongo!


Wimbo wa Salamu zangu uliotungwa na Bi Irene Sanga na kuimbwa naye kwa kushirikiana na Mrisho mpoto umetokea kufunika mno katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania, hasa kutokana na misemo yake isiyochosha kusikiliza!

Hebu usome hapa mashairi yake...
Kiitikio
Taifa liwapo na huzuni lazima wote tufunge mikanda kiunoni ili matanga yaishe upesi, majanga yanapozidi kimo mioyo ya wanadamu huota kutu hizo ni salam zangu...
Pepo hazina sifa ila pawapo Jehanamu, uzuri ni kipimo cha ubaya, kwani kiumbe chenye uhai na mauti huongozwa na tamaa salam zangu kwako eeehh!

Ubeti I:
Mpendwa mjomba tumetenganishwa na ukuta sidhani kama utatembelea tena kama msimu uliopita, japo kwa sasa utakuwa adimu pokea salamu zangu!

Ukienda msibani aliyefiwa utamjua, atakuwa amevaa tofauti na wenzake na machozi yasokauka... Mimi najua ni wewe mfiwa alo na huzuni msiba wetu kuubeba!

Ala moja haikai panga mbili, gimba lisilo akili Waswahili husema ni gogo, taja magogo yote la mbuyu si la mvule, aah funzo la mjinga ni taabu, gome la udi si la mnuka uvundo, isiyokuwasha hujailamba, pokea salamu zangu mjomba!

Ola wendako kabla hujafika, osha uso ndipo ua nje, pa shoka hapaingii kisu, tukifunga mikanda matanga yata isha upesi kwani zindiko la mwoga ni kemi, ukistahi mke ndugu huzai naye, kumbuka vijana ni samadi ya Taifa hili hizi ni salam zangu kwako mjomba!

Mjomba maisha ni sahani iliyojaa kila aina ya uchafu, umeibeba, dudu liumalo usilipe kidole, enda na uchao, usende na uchwao, kichwa cha nyoka hakibandiki mtungi ati, kosa halitengezi kosa , mchunga peku hapendi ila hana viatu, sikufundishi mjomba ila ni salam zangu kwako!

Mwenda mbio kaagana na nyonga, umesha agana na nyonga weye? Usiukubali Utanzania na kutukuza Uingereza, usifikiri kwa lugha za kigeni, fikra sahihi, huja kwa lugha sahihi!

Rushwa, rushwa ni wimbo wa sumu uliotapakaa kwenye ubongo wa kila mwana Taifa hili, tubadilishie wimbo huu tafadhali, turudishie nyimbo zetu za ushujaa, nyimbo za makuzi na jando la Taifa!

Nakuomba jaribu kula majalalani na watoto wa mitaani badala ya kusema this country bwana is very poor? Waonee huruma wajawazito wakiwa wamelala mzungu wa nne kule Amana huku matumbo ya mama hawa yakisubiri mgomo wa madaktari uishe, wengine wakilia kwa kupoteza vichanga vyao

Kiitikio tena!

Ubeti II:
Wapokee masufuria ya moto mama ntilie wakiwa wanafukuzwa na Wagambo wamurike mapolisi wenye madaraka mkononi wakiwahukumu raia kwa makofi kabla hakimu hajasoma hukumu, watoe wafungwa waliofungwa kwa hila na chuki binafsi, sikufundishi mjomba hizo ni salam zangu kwako!

Unakazi mjomba, kumbusha jopo lako wametupima viatu mwaka huu baada ya miaka mitano watatuuliza mlikuwa mnataka viatu vya aina gani?

Maneno mengi hayajengi ghorofa, hili ni ombi langu la mwisho kwako, vibwaya, vibwaya viweke ghalani, siku yake utavikumbuka ili tucheze ngoma yetu wanayoiita ngoma ya kishenzi, visima vya kale havifukiwi mjomba, salamu zangu kwako, ndimi pangu pakavu nakusalimia!

Kiitikio tena!

Filamu ya Kimataifa ya Kanumba kuzinduliwa Dar!


Filamu ya Kimataifa ya Dar 2 Lagos iliyotungwa na kuchezwa na muigizaji mahiri wa filamu nchini Steven Kanumba maarufu kama Kanumba inataraji kuzinduliwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwishoni mwa mwezi huu.
Filamu hiyo inayofungua ukurasa mpya katika anga za filamu nchini, hasa kutokana na kushirikisha wasanii wa mbili tofauti nchi pamoja na kurekodi katika mbili tofauti bila kusahau ndani ya ndege ikiwa angani na kuigizwa kwa umahiri mkubwa na waigizaji hao nyota.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi, mtunzi huyo alisema kwamba filamu hiyo iliyotumia lugha za Kiingereza na Kiswahili ilianza kurekodiwa jijini Dar es salaam kabla ya kwenda kumaliziwa vipande vingine nchini Nigeria kulingana na muongozo wa filamu hiyo.
Akasema kwamba, filamu hiyo imewashirikisha waigizaji wawili toka nchini Tanzania, ambao ni Emmanuel Myamba pamoja naye huku waigizaji toka Nigeria wakiwa Mercy Johnson na Bimbo Akintoe pamoja na washiriki wengine.
Uzinduzi huo utakaofanyika Novemba 30 mwaka huu, unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam sambamba na burudani zingine toka kwa waigizaji mahiri nchini kama Kiwewe, Mtanga, Masele, Matumaini na wengineo pamoja na bendi za African Stars 'Twanga Pepeta' na 'Twanga Chipolopolo'.
Aidha, baadhi ya wasanii wa maigizo toka nchini Nigeria watakakuwemo katika uzinduzi huo ambapo wanaotarajiwa kuwasili nchini katikati ya mwezi huu ni Emanuel Francis, Nkiru Silvanus pamoja na walioshiriki katika 'muvi' hiyo.
Filamu hiyo imeandaliwa na kampuni ya Game 1st Quality ya jijini Dar ambayo ni mmoja wa wadhamini wa uzinduzi huo wakishirikiana na Dotnata Decoration nayo ya jijini Dar.
Wapiga kura wametamka:
Kura zimepigwa kutafuta saa ya mkutano wa kwanza kabisa wa wanablogu na wapenzi wa blogu wa Tanzania. Mkutano utafanyika saa nane mchana saa za Tanzania, Novemba 18, 2006.

Wapiga kura waliochagua saa nane mchana wameshinda. Hakuna masanduku ya kura yaliyoibwa wala kura zilizoharibika. Wala hakuna pingamizi lolote.

Maandalizi ya mkutano yanaendelea katika ukurasa wa wiki ambao utaupata kwa kubonyeza hapa. Tafadhali shiriki kwenye maandalizi. Ukipata tatizo la jinsi ya kuweka maoni yako kwenye ukurasa wa maandalizi ya mkutano, bonyeza hapa usome maelezo mafupi.

Kura 22 zimepigwa kuchagua saa nane mchana kwa saa za Tanzania
Kura 19 zimepigwa kuchagua saa sita mchana kwa saa za Tanzania
·
Hivyo: Mkutano wa wanablogu na wapenzi wa blogu wa Tanzania ni tarehe 18 Novemba, 2006, saa nane mchana saa za Tanzania.

Kama unataka kujua saa nane za mchana Tanzania ni saa ngapi hapo ulipo (kama upo nje ya TanzaMkutano huu utafanyika kupitia teknolojia ya Internet Relay Chat, hivyo utakuwa ni mkutano wa mtandaoni. Bonyeza HAPA uende kwenye tovuti ya mkutano.

Maelezo:

Maelezo haya ni muhimu sana maana usipoyafuata hutaweza kushiriki.
1. Nenda kwenye tovuti ya IRC@Work (http://www.ircatwork.com/)
2. Ukifika hapo utakuta kisanduku kina sehemu tatu.
3. Sehemu ya kwanza inasema Nickname. Andika jina lako kwenye kisanduku hicho.
4. Sehemu ya pili inaitwa Server. Usiandike chochote au kubadili chochote hapo
5. Sehemu ya tatu inaitwa Channel, hapo utaandika: #blogubongo
6. Baada ya kufanya hivyo, bonyeza pale panaposema Login
7. Utakuwa umeingia ndani ya ukumbi wa mkutano.
8. Ukishaingia, upande wa juu kulia utaona majina ya watu wengine walioko ukumbini.

Ukitazama chini kabisa utaona ufito mwembamba ambao ndio utautumia kuandika mchango wako kwenye mkutano. Ukishaandika unabonyeza Enter kwenye kompyuta yako ili mchango wako usomwe.



ILANI

Watu wengi tunajiuliza blogu ni kitu gani? Tunatembelea blogu, tunazisoma, tunashawishika kutaka kuanzisha zetu, ila bado tunakuwa tunajiuliza, “blogu ni nini?” Soma makala alizoandika Mfalme wa Blogu Ndesanjo Macha kujaribu kutoa jibu la swali hili. Makala hizi ziko katika sehemu tatu. Bonyeza hapa.

Pia kuna makala fupi katika Wikipedia ya Kiswahili inayojibu swali: blogu ni nini? Bonyeza hapa uisome.

Wednesday, November 15, 2006

SIKU CHACHE BAADA YA DITOPILE KUTUHUMIWA KUUA!



Kumekuwa na mizaha ya kila aina mara baada ya tukio la mauaji ya dereva wa daladala Hassan Mbonde yaliyofanywa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, ona hii sasa... Eti ndo alama mpya ya barabarani!

Thursday, November 09, 2006

Mama Hambiliki Afariki Dunia!


Mugizaji wa kundi sanaa la Kaole la jijini Dar Mama Hambiliki amefariki kutokana na kuugua maradhi ya moyo yaliyomsumbua kwa miezi miwili kabla ya kuzidiwa Alhamisi iliyopita na kukimbizwa Hospitali ya Mwananyala kwa matibabu zaidi ambapo aliaga dunia juzi usiku
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu Shuruti Saidi (49), siku za hivi karibuni hali ya marehemu mama yao ilianza kubadilika na mara kwa mara alikuwa akilalamika kuhusu ugonjwa wa moyo uliofanya afya yake kuzorota siku hadi siku. .
”Miezi miwili hivi iliyopita mama alianza kuugua maradhi ya moyo na daktari alituambia moyo wake umekuwa mkubwa, hivyo alianza kutumia dawa kabla ya Alhamisi iliyopita kuzidiwa na tulimpeleka wananyamala kwa matibabu zaidi lakini kwa bahati mbaya amefariki,” alisema Shuruti.
Alisema kifo cha mama yao kimeacha pengo kubwa kwa familia hiyo kwa vile alikuwa mhimili kutokana na juhudi zake za kutetea, kulinda na kutoa miongozo thabiti kwa wote.
Msanii huyo aliwahi kuvuma katika sanaa ya uigizaji kabla ya Uhuru na kutamba katika vipindi mbalimbali vya michezo vilivyokuwa vikirushwa hewani na Sauti ya Dar es Salaam (TBC) ambayo baadaye iliitwa Redio Tanzania Dar es Salaam na baada ya kuibuka kwa vituo mbalimbali vya televisheni nchini alijiunga na kundi maarufu la Kaole.
Mungu aiweke mahali pema, roho ya marehemu...amina

Monday, November 06, 2006

Ditopile atuhumiwa kuua!


Mkuu wa mkoa wa Tabora Kapteni Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, ametiwa mbaroni na Polisi kwa tuhuma za mauaji ya raia kwa kutumia bastola yake, jijini Dar es salaam, Tanzania.
Habari kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na kamishina wa Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam, Alfred Tibaigana zinaeleza kuwa Ditopile anatuhumiwa kumuua papo hapo Dereva wa daladala Hassan Mbonde mkazi wa Kawe Mzimuni jijini Dar kwa kumpiga risasi kichwani.
Dito anatuhumiwa kumuua dereva huyo juzi saa 2:30 usiku katika njia panda ya barabara ya Kawe na Bagamoyo, wilaya ya Kinondoni baada ya kuchukizwa na hatua ya gari lake kugongwa kwa nyuma na gari lililokuwa likiendeshwa na marehemu.
Gari lililokuwa likiendeshwa na marehemu ni Isuzu Journey linalofanya biashara ya daladala kati ya Ubungo na Tegeta, huku gari ya Dito ikiwa ni aina ya Toyota Prado iliyokuwa ikiendeshwa na Nassoro Mohamed (42) ambalo lilivunjwa taa ya nyuma katika ajali hiyo.